kaa tayari kwa blog yangu mpya ya fashion JACK255.BLOGSPOT.COM....

SEARCH FOR ANYTHING IN THIS BLOG

Sunday, 21 April 2013

ONGEZEKO LA NAULI LIMEATHIRI SEKTA NYINGI

 movedbc
Utaratibu wa kuongeza nauli kwa magari ya daladala pamoja na mabasi yaendayo mikoani, ulioanza Mei 12 mwaka huu, kwa kiwango kikubwa umeathiri mipango ya bajeti ya mtu mmoja mmoja, familia, vikundi vya kijamii, taasisi pamoja na ufanisi katika utendaji kazi.

Maamuzi ya kupandisha nauli, ambayo yalifanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa  Vyombo vya Usafri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), yamelalamikiwa na wadau wengi kuwa haukuhusisha maoni ya wananchi.

Hakuna mwananchi anayeishi bila kuwa na mipango madhubuti ya matumizi ya fedha, hata wazee huko vijijini hupanga matumizi ya fedha zao kidogo walizo nazo ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku. Na inapotokea bidhaa zilizo muhimu kwao zikapandishwa bei ghafla, lazima mtikisiko wake huathiri mipango yao ya maisha ya kila siku, na inawachukua muda mrefu kuziba athari hizo.

Pamoja na kwamba serikali kupitia kwa Waziri wa Uchukuzi Dk. Mwakyembe iliridhia ongezeko la nauli hizo, akisisitiza kuwa wamiliki wote wa vyombo vya usafiri wawe na tahadhari ya kutojiongezea nauli kiholela, akionya kuwa  wote watakaokiuka watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kunyang'anywa leseni, bado kauli hiyo haimsaidii mlalahoi na mfanyakazi wa kawaida.

Wananchi wa kada mbalimbali wameendelea kulalamika na kudai Sumatra haikuwatendea haki kwa kutowashirikisha katika kutoa mapendekezo ya nyongeza ya nauli hizo. Malalamiko yametolewa na makundi kadhaa kuanzia madereva wa magari ya daladala ambao wamewashutumu wamiliki wa mabasi hayo kwa kuongeza kiasi cha marejesho ya kila siku ambayo ilikuwa shilingi elfu sitini kwa kila siku.

Madereva wa daladala wamedai kuwa wamiliki wa mabasi wanayoyaendesha wamepandisha kiwango cha marejesho kutoka sh.60,000 hadi sh.90,000 kwa kila siku, kiwango hicho wamedai hakina tija kwa upande wao kwani kabla ya hapo walikuwa wakijilipa sh. 80,000, lakini sasa wamepunguza na wanajilipa sh.20,000 tu ili kufidia kiwango anachotakiwa kupelekewa mmiliki wa basi.

Wanafunzi wa ngazi mbalimbali nao wameathirika na ongezeko la nauli hizo kwani baadhi yao wamedai fedha walizokuwa wamezipangilia kwa ajili ya matumizi ya muda maalumu, sasa fedha hizo hazitakidhi na wamelazimika kuahirisha baadhi ya ratiba zao kutokana na kugundua kuwa fedha walizozipangia maalumu kwa kazi za kimasomo hazitoshi tena.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu ambao wengi wao wanasoma kwa kutegemea mikopo ya serikali wamejikuta wakihamisha matumizi ya fedha zilizokasimiwa kwa ajili ya ratiba nyingine na kuzielekeza katika gharama za usafiri, hali ambayo inaweza kuathiri mwenendo wa masomo yao.

Kupanda kwa nauli za daladala hasa katika jiji la Dar es Salaam, kumesababisha hata wajasiriamali wengine kama mamalishe kupandisha bei ya vyakula wanavyoviuza katika magenge yao. Awali walikuwa wakiuza sh.1,500 kwa sahani moja ya chakula, lakini mara tu baada ya kupandishwa kwa nauli nao wamepandisha bei ya chakula hadi kufikia sh.2,000 kwa sahani moja.

Sababu  kubwa waliyoitoa ya kupandisha bei ya chakula ni kutokana na kutozwa bei kubwa ya vyakula wanavyovinunua kutoka katika masoko mbalimbali jijini, na wakadai hawakuwa na njia mbadala ya kufidia tozo wanazozipata kabla ya kuwafikia wateja wao. Baadhi ya mamalishe wamedai kuongeza bei ya vyakula kutokana na gharama kubwa za kuwasomesha watoto ambao kila siku lazima wapewe nauli pamoja na fedha za matumizi wakiwa shuleni.

Ni kweli kuwa walionufaika zaidi na ongezeko la nauli kwa ngazi zote ni wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri. Wanachotakiwa wamiliki hao sasa ni kuboresha huduma za mabasi yao ili yatoe usafiri unaoridhisha. Mabasi mengi yanayotoa huduma katika jiji la Dar es Salaam yamepakwa rangi na yanaonekana kama mapya, kumbe ni mabovu na husababisha usumbufu mkubwa kwa abiria na hatimaye kuongeza foleni barabarani.

Tunashauri Polisi wa usalama barabarani waongeze kasi ya ukaguzi wa mabasi ya daladala na kuchukua hatua madhubuti kwa mabasi yote yanayoonekana kutomudu kutoa huduma, yafungiwe mara moja ili wananchi wanaowajibika kulipa nauli kubwa kwa faida ya wamiliki wa mabasi, wasipate usumbufu wa kukwama njiani kwa visingizio vya ubovu wa basi.

Tunadhani pia serikali inao wajibu wa kuangalia upya mishahara ya wafanyakazi wakati wa sikukuu ya wafanyakazi Mei mosi mwezi ujao ili kuwapunguzia makali na siyo kuwabeba wafanyabiashara ambao wanapata faida kubwa.

Wananchi pia yafaa wanapewa fursa ya kutoa maoni yao kuhusu hatua zozote zinazochukuliwa na mamlaka mbalimbali inapolazimu kuwepo kwa mabadiliko ya gharama za maisha kwa wote, kwani misukosuko inayojitokeza katika maamuzi ya ghafla kiuchumi na ambayo yanawagusa wananchi moja kwa moja, huweza kuathiri kiwango cha uzalishaji na kushusha kiwango cha maendeleo.


CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

VIDEO MPYA YA FABOLOUS ALIYOMSHIRIKISHA CHRIS BROWN




CLICK HERE TO WATCH IT