Kwa mujibu wa gazeti la AS ni kwamba Ronaldo ameiweka sokoni nyumba yake kwa dau la €5.4 million. Jumba hilo la kifahari lenye eneo la mita za mraba 800, huku likiwa na vyumba 7 vya kulalia, mabwawa mawili ya kuogelea na viwanja vya ukubwa wa mita 3,000.
Ronaldo amekuwa hafurahishwi na mbinu za utawala wa Raisi Florentino Perez hasa kwenye suala lake la mkataba mpya, raisi huyo amekuwa akitumia suala la mkataba mpya wa Mreno huyo katika kuwafurahisha mashabiki kuliko mchezaji husika. Leo hii gazeti moja lenye habari za kuaminika la AS Bola la Ureno limeripoti kwamba Ronaldo amekataa kusaini mkataba mpya na Real unaoisha 2015.
David Gill, ambaye ni CEO anayemaliza muda wake Manchester United, mwezi uliopita alikutana na wakala wa Ronaldo Jorge Mendes jijini Madrid kuzungumzia kuhusu dili la kumrudisha Ronaldo Old Trafford wakati wa dirisha la usajili litakapofunguliwa.
Pia katika kuzidi kuzipa tetesi za kurudi kwa Ronaldo Old Trafford - jioni hii akaunti rasmi ya habari ya Manchester United kwenye Twitter alifanya kituko cha ajabu pale ilipoandika taarifa ya kumkaribisha Ronaldo Old Trafford na kuifuta tweet hiyo muda mfupi baadae.