MAMA wa aliyekuwa msanii maarufu Bongo, marehemu Hussein Mkiety ‘Sharo Millionea’, Zainab Mkiety amemkataa mtoto ambaye alipelekewa Tanga na mama yake anayetokea Geita akidai ni damu ya Sharo.
Mtu wa karibu na familia hiyo ameliambia gazeti hili kuwa baada ya msiba kupoa, mama wa mtoto huyo alifunga virago na mwanaye kwa ajili ya kwenda kutembelea kaburi la Sharo na kwenda kujitambulisha kwa bibi wa mtoto.
Chanzo hicho kilieleza kuwa mama mtoto huyo alipofika Muheza jijini Tanga, alipokelewa na watu wa bodaboda ambao walimsindikiza hadi nyumbani kwa mama Sharo.
“Alipofika alipokelewa lakini cha kushangaza mama Sharo alimkataa na kusema marehemu hakuwa na mtoto kwa sababu hakuwahi kumwambia,” alisema sosi huyo.
Ili kupata ukweli wa habari hiyo, paparazi wetu aliwasiliana na mama Sharo kwa simu ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Ni kweli alikuja mwanamke akiwa amebeba mtoto ambaye alijitambulisha kwangu kuwa ametokea Geita.
“Alisema mtoto aliyekuwa amembeba ni wa Sharo lakini nilikataa nikamwambia kuwa mwanangu hakuwahi kuniambia kuwa ana mtoto na nilipowauliza marafiki zake walisema hawana taarifa hizo.
Nisingeweza kumpokea kwa sababu alishajitokeza mwingine na kudai kuwa ana mimba ya mwanangu, baada ya kumkataa mwanamke huyo aliondoka na mpaka leo sina mawasiliano naye.”
Sharo alifariki dunia kwa ajali ya gari Novemba 26, mwaka jana katika Kijiji cha Maguzoni-Soga, Wilaya ya Muheza jijini Tanga.
No comments:
Post a Comment